Mtoto mchanga, Antidius Avitus (miezi minne) amekutwa amefariki dunia na baadhi ya viungo vya mkono wake vikiwa vimenyofolewa huku bibi yake wa kambo akihusishwa.
Mauaji hayo yametokea Nkindo, Kijiji cha Itahwa, Kata ya Karabagaine, Manispaa ya Bukoba.
Akizungumza na Mwananchi Novemba 11, 2024, mama wa mtoto huyo, Dorice Avitusi amesema tukio hilo lililotokea Jumamosi Novemba 9, 2024.
Amesema jana asubuhi alikuwa na mwanawe akiwa mzima na alimwandalia uji kabla ya kwenda naye kanisani kufanya usafi.
Anasema alirejea nyumbani mchana akiwa amembeba mgongoni akiwa amelala na akapitiliza kwenda kumlaza chumbani.
Akisimulia huku akibubujikwa machozi, Dorice amesema alienda dukani na aliporudi akaendelea kupika chakula cha mchana huku mtoto akiwa kalala.
“Nilipomaliza kupika tukala na ilipofika saa tisa nikasikia mtoto analia nikaenda kumchungulia dirishani, nikaona bado amesinzia, nikaendelea na shughuli zangu,” anasimulia Dorice.
Anasema alipomaliza shughuli zake alienda kumuangalia tena ndipo akakuta chandarua na mashuka yakiwa na madoa ya damu, alipomfunua mtoto alikuwa anatokwa na povu puani na mdomoni na mkono ulikuwa umechunwa ngozi na baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa.
"Niliogopa sana nilipoona mwanangu yupo katika hali hiyo; mapovu yalikuwa mengi puani na mdomoni, na mwili wake ulikuwa kama umepakwa dawa za kienyeji. Nilianza kumtafuta mume wangu kwa simu na alifika na kuanza kuwasiliana na majirani," amesimulia mama huyo. (Soma Zaidi>)