Na Stephano Mango, Songea
WAKAZI wa Mtaa wa Luwawasi Mkuzo Manispaa ya Songea wameishukuru Serikali kupitia kwa MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) kwa kutatua changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama iliyokuwa ikiwakabili kwa mda mrefu.
Wananchi hao Musa Aziz, Janeth John na Skora Mwingira wameeleza namna walivyokuwa wanapata changamoto yakufuata maji umbali mrefu huku maji hayo yakiwa sio safi na salama pamoja na kusababisha ndoa zao kuteteleka kutokana na wakina mama kutumia mda mrefu kutafuta maji.
Wamemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuwawezesha kutatua changamoto hiyo na sasa wanapata kwa urahisi zaidi huku wakiepukana na magojwa ya mara kwa mara yaliyokuwa yanasababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.
Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA Mhandisi Patrick Kibasa alisema kuwa Mamlaka imeamua kupeleka mradi huo wa maji katika Mtaa huo ili kutimiza malengo ya Serikali ya kumtua Mama ndoo kichwani
Mhandisi Kibasa alisema kuwa Wananchi hao walikuwa wanapata adha kubwa sana ya maji hivyo mradi huo ni ukombozi mkubwa sana kwao.
Aliwataka Wananchi hao kutoa ushirikiano mkubwa sana kwa mafundi wanaofanya maunganisho ya maji ya mradi huo ili wakamilishe kwa wakati na kuwataka kutunza miundombinu ya maji ili iweze kuwa na manufaa zaidi kwao.
Aidha, wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa mafundi wa uchimbaji mitaro ya maji kwa kuepuka kelele au migogoro inayoweza jitokeza kwa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wakati wateja wapya wanaunganishiwa huduma hiyo.
Afisa Mawasiliano na uhusiano kwa umma SOUWASA Paul Mandia amesema kwa Manispaa ya Songea wanatarajia kupita sehemu zote korofi ambazo ni kikwazo kwa wananchi kwa kuzungumza nao na kutatua kero zao.
Mandia amewasihi wananchi kutoa ushirikiano kwa mamlaka pindi wanapopata changamoto kwa kupiga simu ya ofisini kwani Souwasa inafanya kazi masaa 24.