Wanafunzi 20 Wanusurika Kifo Ajali ya Basi Mtwara

Adimin
0

 Wanafunzi 20 wa shule ya msingi Salem, walimu Wawili na Dereva wamejeruhiwa katika ajali iliyohusisha Basi la shule hiyo kugongana na Gari la Jeshi, mtaa wa Magomeni Migomigo, Manispaa ya Mtwara Mikindani.


Kwa mujibu wa mashuhuda, ni kwamba ajali hiyo imetokea Novemba 28, 2024 majira ya saa 12 jioni, ambapo wanadai chanzo chake ni gari ya jeshi lililokuwa linatoka mjini kwenda uelekeo wa Naliendele ambalo lilikuwa linajaribu kulivuka Lori lililokuwa limeegeshwa, ndipo likakutana na basi hilo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula, Dokta Zawadi Bwanali, amethibitisha kuwapokea majeruhi 23 wa ajali hiyo, ambapo kati yao, wanafunzi ni 20, walimu Wawili pamoja na Dereva.

Amesema, majeruhi wameanza kupokelewa hospitalini hapo majira ya saa 1 usiku na kuanza kupatiwa huduma, ambapo mpaka kufikia majira ya saa 5 usiku, majeruhi Tisa wakaruhusiwa na kusalia na wengine 14.

“Tuna wagonjwa wawili sasaivi wanaingia ‘Theatre’ kwa maana ya mwanafunzi mmoja na mwalimu mmoja. Huyu mwalimu alivunjika mguu, lakini pia mwanafunzi alivunjika mguu na alipata matatizo kwenye ubongo, kwahiyo huyu mwanafunzi sasahivi yupo ‘Theatre’ lakini akishatoka huyu mwanafunzi mwalimu pia ataingia kwenda kufanyiwa matibabu kule ‘Theatre’.” Amesema Dkt. Zawadi.

Ameongeza kuwa, majeruhi mmoja amekimbizwa hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kusini kwa ajili ya kwenda kufanyiwa vipimo vya CT-Scan.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top