Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita amesema Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa wa ACT, Abdul Nondo, alitekwa alfajiri December 01,2024 katika stendi ya Magufuli, Mbezi Luis Jijini Dar es salaam na kisha kutupwa Coco Beach, Dar es salaam ambako baadaye Wasamaria wema walimsaidia na kumpeleka Makao Makuu ya Chama hicho Magomeni Jijini Dar es salaam akiwa na majeraha na kisha akapelekwa Hospitali huku Kiongozi Mstaafu wa ACT, Zitto Kabwe akisema Nondo mwenyewe akipata nafuu atasimulia tukio zima lilivyotokea.
Akiongea usiku wa kuamkia leo, Hospitalini ambako Nondo amelazwa, Mchinjita amesema “Nondo alitekwa alfajiri ya jana pale stendi ya Magufuli, baada ya ufuatiliaji tukabaini gari iliyomteka ipo Gogoni Kituo cha Polisi lakini Polisi wakakataa kuwa hawakuwa na Nondo, usiku saa nne tukapata taarifa Nondo ametupwa Coco Beach na Wasamaria Wema wakamleta ofisi ya Chama Walinzi wetu walituambia aliletwa na Bajaji”
“Nondo amepigwa sana amepata majeraha makubwa hasa maeneo ya miguu, kifua, mgongo na mikono na alifungwa kwa muda mrefu inaonekana mikono yake imevimba amekuwa akijieleza kwa tabu sana, tumemleta Hospitali, Madaktari wametueleza taarifa za awali za hali yake, Mtu wa kwanza kabisa alitupa taarifa kuhusu kutekwa kwa Nondo alikuwa ni John Mnyika (Katibu Mkuu CHADEMA)”
Kwa upande wake Zitto Kabwe amesema “Makamu Mwenyekiti amewaeleza kwa kifupi, muhimu ni Abdul apate matibabu, naamini yeye mwenyewe akipata nafuu atakuwa na uwezo wa kueleza tukio zima nini kilitokea ili iwe funzo siku za usoni jinsi gani tunaweza kukabiliana na matukio kama haya, tulikuwa nae kwenye kampeni hatukuona tishio wala jambo lolote Abdul kuingizwa kwenye mtihani huu”