jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara linamshikilia dereva wa bajaji, Paskali Lori Tluway, mwenye umri wa miaka 32, mkazi wa Mtaa wa Negamsi, wilayani Babati, Manyara, kwa tuhuma za kumwingilia kinyume cha maumbile mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka minane. Tukio hilo la ajabu na la kusikitisha lilitokea Novemba 23, 2024, saa 10 jioni katika Mtaa wa Negamsi, Kata ya Bagara, Halmashauri ya Mji wa Babati.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kija Mkoy, mama wa mtoto huyo alikuwa nje ya nyumba wakati mtoto wake akiwa ndani na baba yake.
Amesema mwanamke huyo alipofungua mlango, alikuta mume wake akimtendea ukatili mtoto wao, akapiga kelele kuomba msaada.
Majirani walikusanyika na kumshauri kumfungia mtuhumiwa ndani na kutoa taarifa kwa jeshi la polisi. Uchunguzi wa awali, ukijumuisha uchunguzi wa daktari, umeonesha kuwa ni kweli mtoto alitendewa unyama huo, na kwamba jalada lipo tayari kwa hatua zaidi. Mtuhumiwa huyo anadaiwa kusema maneno ya kibangibangi kwamba amemwanzishia ili akikua aendelee.