Na Stephano Mango, Nyasa
WANANCHI wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma wamehamasishwa kujiunga na Chuo cha ufundi stadi VETA Nyasa ili waweze kupata elimu ya ujuzi wa fani mbalimbali.
Wito huo umetolewa na Mkuu Wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafari ya kwanza ya Chuo cha Ufundi Stadi Veta Nyasa
Magiri amewataka wananchi wa Wilaya ya Nyasa kusoma chuo cha VETA Nyasa kwa lengo la kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri, na kuongeza kipato kwa mtu mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla.
Uwezo wa Chuo hiki ni kuchukua wanafuznzi zaidi ya 160, lakini mpaka sasa chuo hiki kinadahili wanafunzi 80 hivyo basi tunatakaiwa kutumia fursa hii kupata ujuzi.
Magiri ameongeza kuwa Elimu ya Ufundi haina mipaka ya umri cheo hivyo basi wananchi wote tunatakiwa kupata ujuzi ambao utatusaidia kuongeza kipato cha ziada na kuboresha maisha yetu,
“ Nimejipa ubalozi wa kukitamgaza Chuo cha Ufundi Stadi Veta Nyasa, Sijaridhika na jinsi wananyasa tunavyokitumia Chuo hiki kwa kuwa bado tunakuwa na nafasi nyingi za kusoma lakini hatutaki kuleta vijana wetu.
Nachukua fursa hii kuwataka viongozi na wananchi kwa ujumla wake kuhakikisha tunawaleta vijana wetu katika chuo hicho ili wapate ujuzi wa Umeme,ushonaji,Magari, ujenzi, Useremala na Udereva.
Aidha amewapongeza wanafunzi ambao walikuwa wanaonyesha jinsi mashine zinavyofanya kazi katika Karakana ya Ufundi magari, Umeme, na Ujenzi na kusema kuwa Chuo hiki kinatoa elimu bora na wanachuo wameiva tayari kabisa kwenda kujenga Taifa la Tanzania.
Aidha amewasihi wahitimu kwenda vijijini na kutumia ujuzi wao kwa kuanzisha vikundi kwa kufanya shughuli walizosomea na Serikali itawaunga mkono kwa kuwakopeshha asilimia kumi ya mapato, badala ya kwenda mijini kupoteza muda.
Awali Mkuu wa Chuo hicho ameiomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya umeme kwa kuwa kuna mashine za kisasa zinazotumia umeme mwingi zaidi ombi ambalo limepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa na limeanza kufanyiwa kazi.
Aidha amewataka wazazi walezi kuwaleta wanafunzi katika chuo hicho kwa kuwa bado kinanafasi za kutosha kuwapa ujuzi wakazi wa Wilaya ya Nyasa na maeneo mbalimbali
Kwa upande wao wahitimu wameridhishwa na elimu inayotolewa chuoni hapo.