Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza, imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela Amos John Malaki (30), mkazi wa Kijiji cha Soswa, baada ya kupatikana na hatia ya kuwajeruhi watu wawili kwa kuwang'ata kwa meno.
Mshtakiwa amefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza leo, Februari 17, 2025, na kusomewa mashtaka katika kesi ya jinai namba 4079/2025. Jamaa hakutaka kuisumbua mahakama na hivyo, amekiri makosa yake.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nyamhanga Tissoro, ameieleza mahakama kuwa mnamo Januari 8, 2025, saa 5:57 usiku, mshtakiwa alimlima jino kwenye jicho Regina Thomas.
Katika tukio jingine, Januari 9, 2025, saa 6:01 usiku, njemba huyo akamng'ata na kukiondoa kabisa kidole gumba cha mkono wa kulia cha Mashaka Idd Daudi, aliyekuwa akijaribu kusuluhisha ugomvi. Mahakama imeambiwa kwamba matukio hayo ni kinyume na Kifungu cha 225 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya 2022