Huduma ya Kitaifa ya Polisi nchini Kenya(NPS) imetoa taarifa kuhusu ajali mbaya iliyohusisha msafara wa Rais William Ruto.
Mnamo Alhamisi, Machi 13, raia mmoja wa kigeni ambaye hajatwa wa nchi gani aligongwa na kuuawa na gari lililokuwa likiendeshwa kwa kasi lililounganishwa na msafara wa rais kando ya Barabara ya Ngong.
Katika taarifa, Msemaji wa NPS Muchiri Nyaga alisema uchunguzi umeanzishwa kufuatia ajali hiyo.
"Kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea katika uwanja wa Adams Arcade kando ya Barabara ya Ngong, iliyohusisha magari ya serikali na kusababisha kifo cha mtembea kwa miguu ambaye ni raia wa kigeni, Huduma ya Kitaifa ya Polisi inashughulikia suala hilo, na uchunguzi umeanza," Muchiri alisema.
Muchiri alimtaka Mkenya yeyote aliyeshuhudia ajali hiyo kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu ili kusaidia katika uchunguzi.
"Tunahimiza mtu yeyote aliye na taarifa zinazoweza kusaidia katika uchunguzi kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu au kupitia nambari yetu ya bure ya 999, 911, 112," NPS ilisema.