Binti aliyedaiwa kutekwa akiwa na mdogo wake na kusababisha vurugu zilizopelekea kifo cha kijana mmoja katika mjini mdogo wa Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu, na kisha kupatikana akieleza kuwa alitoroka nyumbani yeye mwenyewe akiwa pamoja na mdogo wake, amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu ACP. Edith Swebe amesema kuwa binti huyo aitwaye Rahma Hamis (19), ambaye ni mkazi wa Bukombe ambaye alisadikiwa kuwa ametekwa na kusababisha vurugu zilizopelekea kifo cha mtu mmoja, majeruhi na uharibifu wa kituo cha Polisi Lamadi pamoja na uharibifu wa mali za watu tukio lilotokea Agosti, 2024 amehukumiwa kifungo cha miaka saba (7) mnamo Aprili 03, 2025 katika mahakama ya hakimu mfawidhi wa mkoa wa Simiyu.
Kamanda Swebe amesema kuwa Rahma Hamis amehukumiwa kifungo cha miaka saba kwenda jela kwa kukutwa na hatia ya kuiba mtoto aitwaye Stephano Godfrey, chini ya kifungu cha 169 kifungu kidogo (1) (a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022, ambapo hukumu hiyo imetolewa na hakimu mfawidhi mkoa wa Simiyu Mheshimiwa Martha Maumbuga.
Katika hatua nyingine kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeno mbalimbali ya mkoa huo pamoja na kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.