Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema inatarajiwa kuketi Juni 03, 2025 ikiwa na ajenda kuu ya kujadili taarifa na maamuzi ya Msajili wa Vyama vya siasa iliyositisha ruzuku kwa Chama hicho pamoja na kusisitiza kutoutambua uongozi wa sasa wa Chama hicho uliopatikana kupitia Kamati kuu ya Januari 22, 2025.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche amebainisha hayo Jumanne Mei 28, 2025 akiwa Jijini Arusha kwenye muendelezo wa ziara ya No reforms, No election, akibainisha kuwa katika kikao hicho ndipo maamuzi ya Chama yatafakiwa na kutoa muelekeo wa kule Chadema itakapokuwa inaelekea.
"Tumeitisha Kamati kuu ya Chama Tarehe tatu, tutarudi kujadili barua ya Msajili na kutoa mwelekeo wa nchi wapi tunaelekea. Mimi jana nimeambiwa kuwa siku zangu zinahesabika, niwaambie watu wa Arusha, sitakimbia nchi hii hata kwa dakika moja, nitakuwepo na hata kama damu yangu itamwagika tusirudi nyuma, tusonge mbele mpaka tutakapopata mabadiliko kwenye nchi hii." Amebainisha Kiongozi huyo.
TAZAMA VIDEO YA HECHE HII HAPA
Heche pia amebainisha uwapo wa majaribio mengi ya kutaka kuiua Chademaz akisisitiza kuwa Chadema haitokufa kutokana na mapwnzi makubwa ya wananchi sambamba na matumaini yao kwa Chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Ujio wa Kikao cha Kamati kuu unafuatia barua ya Jana Mei 27, 2025 iliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini ambapo kulingana na Mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 18(6) cha sheria ya Vyama vya siasa, alitangaza kusitisha kutoa ruzuku kwa Chadema hadi pale watakapotekeleza maelekezo ya Ofisi ya Msajili akidai kuwa kwazaza Chadema haina Viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na marejesho ya fedha hizo za Umma.
Hatua ya Ofisi ya msajili wa Vyama vya siasa ilifikiwa mara baada ya kueleza kuwa Chadema imekaidi mara kadhaa maamuzi ya Ofisi ya msajili, ikiwemo taarifa ya Mei 25, 2025, ambapo Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche akisoma Maazimio ya Kamati kuu ya Chama, alieleza kuwa maamuzi na maelekezo ya Msajili wa Vyama vya siasa kuhusu malalamiko ya Bw. Lembrus Mchome ni batili na hawatoyafanyia kazi.