Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. @mwigulunchemba (Mb), amewasilisha Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali, ambapo ameliomba Bunge ridhaa ya kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 56.49 kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.
Dkt. Nchemba ameomba ridhaa hiyo bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/26, ambapo bajeti hiyo inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani ya shilingi trilioni 40.47, misaada shilingi trilioni 1.07 na mikopo ya shilingi trilioni 14.95.
‘‘Kati ya mapato ya ndani yanayotarajiwa, mapato ya kodi ni shilingi trilioni 32.31, mapato yasiyo ya kodi shilingi trilioni 6.48, na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 1.68. Aidha, mikopo inajumuisha shilingi trilioni 6.27 kutoka vyanzo vya ndani na shilingi trilioni 8.68 kutoka vyanzo vya nje’’, alifafanua Mhe. Nchemba.
Alieleza kuwa makadirio ya matumizi ya Serikali ya shilingi trilioni 56.49 kwa mwaka 2025/26 yanajumuisha Stahiki za watumishi na michango ya pensheni (Serikali Kuu) shilingi trilioni 9.17 pamoja na ununuzi wa bidhaa na huduma shilingi trilioni 5.58.
Aliongeza kuwa matumizi mengine ni malipo ya riba za mikopo shilingi trilioni 6.49; na ruzuku kwa taasisi za Serikali, mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 22.17 na shilingi trilioni 7.72 kugharamia malipo ya mtaji kwa deni la ndani na nje.
‘‘Katika Mwaka wa Fedha 2025/26 Serikali inatarajia kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2025 kutoka ukuaji wa asilimia 5.5 mwaka 2024, kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 - 5.0 katika muda wa kati’’, alifafanua Mhe. Nchemba.
Aidha, Dkt. Nchemba alisema Serikali inatarajia kuongeza Mapato ya ndani kufikia asilimia 16.7 ya Pato la Taifa mwaka 2025/26 ikilinganishwa na asilimia 15.8 mwaka 2024/25 na mapato ya kodi kufikia asilimia 13.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025/26 kutoka asilimia 12.8 mwaka 2024/25.