Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limeeleza kupatikana kwa mabaki yanayodaiwa kuwa ni ya mwili wa Sadick Sanga (52) aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Utengule wilayani Kalambo aliyeripotiwa kupotea Machi, 2025.
Jeshi hilo limeeleza kuwa linawashikilia pia watu wawili kwa tuhuma za mauaji hayo kwa kumpiga na kitu kizito kichwani.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Jumatano Juni 25, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la polisi SACP, Shadrack Masija amewataja watu hao wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo kuwa ni Edward Yohana (30) na Shadrack Bernard (27) wote wakazi wa Kijiji cha Utengule.
“Sadiki aliripotiwa kupotea Machi 2025, tulikuwa tunashirikiana na ndugu kwa lengo la kumtafuta, Juni 20 tulipata mabaki kwa maana ya fuvu la kichwa cha binadamu pamoja na mifupa lakini kulikuwa na nguo ambayo ilitambuliwa na ndugu zake kwamba ni nguo yake na kwa sababu ni kijijini watu wanamuona akiiva siku zote kwa hiyo tukaamini kwamba mabaki yale yalikuwa ni ya Sadiki," amesema.
Kamanda Masija ametaja chanzo cha mauaji hayo kuwa ni wivu wa mapenzi ambapo marehemu alidaiwa kuwa na mahusiano na mke wa mmoja wa watuhumiwa hao na hivyo walipanga kulipiza kisasi kwa kumuadhibu.
Jeshi la polisi linawataka wananchi waache vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watumie njia sahihi zisizoleta madhara kwa jamii.
Pia, jeshi hilo limetoa wito kwamba taarifa za watu waliopotea zifikishwe polisi na wananchi watoe ushirikiano wa kutosha kwa jeshi la polisi kumtafuta aliyepotea.