Mashine kutumika kuongeza virutubisho vya lishe mkoani Njombe

Adimin
0

 Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda, katika kikao maalum kilichofanyika tarehe 25 Juni 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe. Kikao hicho kililenga kujadili kwa kina hali ya lishe mkoani humo, hususan kwa watoto, wanawake wenye umri wa kuzaa na vijana balehe, kwa lengo la kupunguza tatizo la udumavu na kuimarisha afya ya jamii.



Katika hotuba yake, Mhe. Sweda aliwaeleza washiriki kuwa Mkoa wa Njombe unaendelea kutekeleza Mkataba wa Lishe, ambapo jumla ya mashine 708 za kusaga unga wa mahindi zilibainika kuwepo, lakini ni mashine 17 pekee ndizo zilizoanza kuongeza virutubishi muhimu kwenye unga. Alieleza kuwa hali hiyo bado inakabiliwa na changamoto za uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa virutubishi, pamoja na usimamizi hafifu wa kanuni za urutubishaji wa vyakula.

Aidha, alifafanua kuwa Mkoa ulipokea mashine mpya nane (8) za kuongeza virutubishi kutoka Wizara ya Afya, zilizokabidhiwa kwa Halmashauri mnamo tarehe 6 Juni 2025. Aliagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha mashine hizo zinafungwa na kuanza kazi mara moja, huku wakitenga bajeti kwa ununuzi endelevu wa virutubishi ili kuhakikisha wananchi wanapata unga wenye virutubishi bora unaosaidia kupunguza udumavu.

Mhe. Sweda alihitimisha kwa kusisitiza kuwa mafanikio ya kupambana na hali duni ya lishe yanahitaji mshikamano wa pamoja kati ya serikali, jamii na wadau wa maendeleo. Alitoa wito kwa viongozi wa halmashauri kuwapatia elimu wamiliki wa mashine na kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha urutubishaji wa vyakula unafanyika kwa viwango vinavyotakiwa kwa ustawi wa jamii ya Mkoa wa Njombe.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)
To Top