Klabu ya Yanga SC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2024/25 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC, katika mchezo wa kukata na shoka uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na nyota wake mahiri Pacome Zouzoua na Clement Mzize, ushindi huo ukiwa ni wa tano mfululizo dhidi ya Simba katika michezo ya hivi karibuni.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 82, ikimaliza msimu ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi huku Simba ikishika nafasi ya pili kwa alama 78.
Huu ni ushindi wa tano mfululizo wa Yanga dhidi ya Simba SC, rekodi ambayo inazidi kuimarisha historia yao ya mafanikio katika mechi za watani wa jadi.
Rais Samia Apongeza Mafanikio ya Yanga
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa salamu za pongezi kwa klabu ya Yanga kwa kutwaa ubingwa wa 31 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, na wa nne mfululizo.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Rais Samia ameandika:
Ushindi huu wa kihistoria unaifanya Yanga kuendelea kuwa klabu yenye rekodi bora zaidi nchini, huku wakimaliza msimu kwa kishindo na kufurahisha mashabiki wao lukuki ndani na nje ya Tanzania.