Mkutano wa hadhara uliohutubiwa na viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, John Heche umechangia kampeni ya 'Tone Tone' Sh2.7 milioni.
Makamu Nwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Kamati Kuu ya Chadema, Boniface Jacob amesema kiasi hicho kimekusanywa baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Dodoma ikiwa ni mchango mkubwa tangu chama hicho kilipoanza ziara ya mikutano ya hadhara miezi mitatu iliyopita.
Viongozi wa chama hicho tayari wamefanya ziara katika Kanda za Nyasa, Kusini, Victoria, Serengeti, Kaskazini na sasa wako Kanda ya Kati inayoundwa na mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida.
"Kwa mamlaka niliyopewa na Kamati ya Fedha ya Changizo la 'Tone Tone' napenda kutangaza kuwa katika mkutano wa leo Dodoma Mjini uliohutubiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika tumekusanya Sh2,766, 350," amesema Jacob katika taarifa yake
Amesema makusanyo hayo kwa sasa ndio makubwa ikilinganishwa na rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na mkutano wa Arusha Mjini ambako chama hicho kilikusanya zaidi ya Sh1.3 milioni.
"Fedha tuliyokusanya Dodoma mjini ni zaidi ya jumla ya fedha zote tulizopata katika mikutano ya Arusha Mjini na Moshi Mjini zilizofikia zaidi ya Sh2.4 milioni," amesema Jacob.
Amesema mkutano wa Arusha Mjini zilikusanywa zaidi ya Sh1.3 milioni, pia chama hicho kilikusanya zaidi ya Sh1.09 milioni katika mkutano wa Moshi Mjini.
Heche amesema mwamko na mwitikio wa umma kukichangia chama hicho ni ishara ya kukubalika kwa ajenda ya kudai mabadiliko kupitia kampeni ya 'No reforms, no election' inayodai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi kuweka sawa uwanja wa siasa kwa wagombea na vyama vyote vya siasa.