Wanachama wa chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Makete wamepiga kura za maoni kuwachagua wawakilishi katika chaguzi za serikali za mitaa kupitia chama hicho.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa CCM wilaya ya Makete Daniel Mhanza amesema baada ya mchakato huo kukamilika katika matawi kutakuwa na mchakato wa mapendekezo na uteuzi kwa wagombea wote na kupitia vikao vya chama vitawateua wawakilishi wa chama hicho huku katibu wa itikadi na uenezi CCM wilaya Yusuph Kisimbilo akisema wanachama wakumbuke kuwa hizo ni kura za maoni na uchaguzi kamili unakuja hivyo wajiandae kwenda kupiga kura wakati ukiwadia.
Katibu wa CCM kata ya Tandala Baraka Ilomo amesema katika kijiji cha Tandala aliyeongoza ni Yusuph Ilomo,kijiji Cha Ikonda ni Alexander Mbilinyi,kijiji cha Ihela ni Regina Mgeni na kijiji cha Usagatikwa ni Ibrahimu Sanga.
Awali katika tawi la Tandala wagombea wakaeleza vipaumbele vyao kuwa watahakikisha wanasimamia ujenzi wa zahanati ili kijiji hicho kipate maendeleo zaidi.
Altini Sanga ametangaza matokeo katika tawi la Tandala na kueleza kuwa mchakato umekuwa na mvuto wa kipekee huku wagombea wakieleza kuwa watashirikiana kwa pamoja baada ya uteuzi wa chama kuelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.
Chama cha Mapinduzi CCM Oktoba 23,2024 kimeendesha zoezi la kupiga kura za maoni katika matawi yote Tanzania bara ili kuwapata watakaokiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27,2024.