Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ametangaza mpango mkubwa wa kuwanufaisha zaidi ya kaya 930 katika Jimbo la Lupembe, Wilaya ya Njombe, kupitia mradi wa miche ya parachichi.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mhe. Mtaka aliweka wazi kuwa mradi huo utalenga kaya masikini zinazopokea msaada kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Jamii (TASAF).
Kaya hizo zitapatiwa miche 10 ya parachichi kila moja, ambapo inatarajiwa kwamba baada ya miaka mitatu miche hiyo itaanza kuzalisha matunda. Mradi huo una malengo ya kuinua hali za kiuchumi za wanufaika, kupunguza umasikini, na kuboresha maisha yao kupitia kilimo cha mazao yenye soko la kimataifa.
"Tunaamini kuwa kupitia mradi huu wa parachichi, kaya hizi masikini zitaanza kuona mabadiliko ya kiuchumi baada ya miaka mitatu tu. Parachichi lina thamani kubwa katika soko la ndani na nje ya nchi, na tunataka kila mkulima anufaike na fursa hii ya kimataifa," alisema Mhe. Mtaka.
Aliongeza kuwa mradi huu ni sehemu ya jitihada za Mkoa wa Njombe za kuhakikisha kuwa kaya maskini zinajitegemea kupitia miradi ya kilimo. "Kupitia parachichi, kaya hizi zitaweza kuongeza kipato chao, kujenga uchumi wa familia zao, na kuondokana na umasikini wa muda mrefu," alieleza.
Miche hiyo inatarajiwa kuanza kuzaa matunda ndani ya miaka mitatu, na faida zake ni kubwa. Wananchi wa Lupembe watapata soko la uhakika la parachichi, kwani zao hili limekuwa na mahitaji makubwa kwenye masoko ya kimataifa. Hali hii itasaidia kuongeza kipato cha familia na kuboresha hali ya maisha katika vijiji mbalimbali.
Mradi huu ni mfano mzuri wa namna serikali ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyowekeza katika maendeleo ya wananchi kupitia sekta ya kilimo, ikiwa ni jitihada za kupunguza umasikini na kuinua uchumi wa kaya maskini.