Tanesco Ruvuma Wajikita kutoa Elimu kwa Wananchi Kuhusu Mradi wa Umeme

Adimin
0

Na Stephano Mango,Songea 

TANESCO Mkoa wa Ruvuma imejikita zaidi katika kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya miji na vijijini kabla na baada ya kuanzisha miradi ya umeme, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanahusishwa kikamilifu katika mchakato mzima wa utekelezaji wa miradi hiyo. 



Hii ni sehemu ya juhudi za shirika la umeme kuhakikisha kuwa wakazi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu hatua zinazochukuliwa na Tanesco na michakato yote inayohusiana na umeme.


Hayo yameelezwa na Mhandisi Malibe Boniphace kutoka Tanesco Mkoa wa Ruvuma alipokuwa akizungumza na wakazi wa mkoa huo mbele ya Waandishi wa Habari 


Mhandisi Boniphace alieleza kuwa, moja ya vipaumbele vya shirika ni kufanya tathmini ya kina kabla ya kupeleka miradi ya umeme, ambapo hufanywa utafiti ili kubaini kama maeneo husika hayana huduma ya umeme kabisa au kama huduma hiyo inahitaji kuboreshwa.



Alisema lengo letu ni kuhakikisha kwamba huduma za umeme zinawafikia wananchi kwa usawa, na hii inatokana na bajeti ya fedha inayopatikana kwa kila kipindi.


"Serikali imejizatiti kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata huduma hii muhimu,” alisema Mhandisi Boniphace.


Pia, Mhandisi Boniphace alibainisha kuwa, Tanesco ina mikakati ya kuwafikia wananchi katika ngazi za vijiji na mitaa, ambapo wataelimishwa kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme pamoja na michango inayohusiana na miradi ya umeme katika maeneo yote yaliyopitiwa na miradi hiyo.


Aidha Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja kutoka Tanesco Mkoa wa Ruvuma, Alan Njiro, alizungumzia changamoto za uchomaji wa mashamba maeneo yaliyopitiwa na nguzo za umeme, na athari zinazoweza kutokea kutokana na hilo, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wateja kukosa huduma ya umeme. 


Alisisitiza kuwa ni jukumu la wananchi kulinda miundombinu ya umeme ili kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa usalama na uhakika.


Afisa Njiro aliongeza kuwa, wananchi wanapaswa kuwa makini na wahalifu wanaoweza kujitokeza katika maeneo yao, wakijitambulisha kama wafanyakazi wa Tanesco na kudai malipo kwa ajili ya kuunganishiwa umeme. 


Alifafanua kuwa utaratibu wote wa malipo ya kuunganishiwa umeme unafanyika kwa njia ya simu ya mkononi, na malipo ya serikali hufanywa kwa kutumia namba za kumbukumbu (control number).


Alisema wananchi wanapaswa kuwa na ufahamu kwamba malipo yote ya umeme yanapangwa kwa njia ya simu, na siyo kupitia fedha taslimu kwa wahudumu wa nje.


 Tunatoa wito kwa wananchi kuwasiliana moja kwa moja na ofisi za Tanesco au kupiga simu ili kuepuka kudanganywa na matepeli,” alisema Afisa Njiro.


Kwa kumalizia, viongozi hawa wa Tanesco walisisitiza kuwa jukumu lao ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora ya umeme, lakini pia wanapata elimu ya kutosha kuhusu miradi hiyo na hatari zinazoweza kujitokeza ikiwa miundombinu haitalindwa na wananchi. 


Tanesco inaendelea kuhakikisha kuwa huduma za umeme zinafikishwa kwa usalama na kwa manufaa ya kila mkoa, ikiwa ni sehemu ya kukuza maendeleo ya taifa.

MWISHO

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

JIUNGE NA IDAWA MEDIA SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Idawa Media Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top