Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa benki ya Credit Suisse, Tidjane Thiam ameukana uraia wake wa Ufaransa ili kutimiza masharti ya kushiriki katika uchaguzi wa urais wa Ivory Coast mwezi Oktoba.
Mwaka 2023, Thiam alichaguliwa kuwa kiongozi wa PDCI, moja ya vyama vikuu vya upinzani nchini Ivory Coast, na kumfanya kuwa mgombea wake.
Katika video iliyowekwa kwenye mtandao wa Facebook siku ya Ijumaa, Thiam alisema amewasilisha ombi la kurudisha hati yake ya kusafiria ya Ufaransa, ili kubaki kuwa raia wa Ivory Coast pekee wakati wa uchaguzi.
"Ninasisitiza upya ahadi yangu ya kufanya kazi kwa ajili ya mabadiliko ya kweli nchini Ivory Coast, ili hali ya maisha ya watu wa Ivory Coast iboreke. Hilo ndilo tunalopigania," alisema.
Thiam, 62, aliwahi kuwa waziri nchini Ivory Coast chini ya Rais wa zamani Henri Konan Bedie. Aliondoka katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi baada ya kuondolewa madarakani kwa Bedie katika mapinduzi ya kijeshi ya 1999 na kufanya kazi katika kampuni ya ushauri ya McKinsey, na kampuni ya bima ya Aviva and Prudential, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Credit Suisse mwaka 2015.
Alirejea Ivory Coast na kuingia katika kinyang'anyiro cha uongozi cha chama cha PDCI - chama cha rais wa kwanza wa nchi hiyo, Felix Houphouet Boigny.
Rais Alassane Ouattara, 83, ameashiria kuwa atagombea muhula wa nne, uamuzi ambao huenda ukakabiliwa na upinzani kutoka vyama vya upinzani, ambavyo vilipinga kugombea kwake muhula wa tatu mwaka 2020.