Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Pendo Paul, mkazi wa Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu, ameeleza kuwa ana mashaka na usalama wake baada ya kukataa kutekeleza ombi la uhalifu dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Kisesa Mhe. Luhaga Mpina
Kwa mujibu wa Pendo, amesema mnamo Machi 6, 2025, majira ya saa 12 jioni, alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Mussa Mbuga, ambaye alimuuliza kuhusu uzoefu wake katika Jeshi la kujenga Taifa na matumizi ya silaha.
Baada ya kuthibitisha kuwa ana uzoefu wa miaka miwili, Mbuga alidaiwa kumpa ofa ya kufanya shambulizi dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina, akiahidi kumlipa kiasi chochote cha fedha atakachotaka.
"Nikamwambia siwezi kufanya kazi haramu kama hiyo, kama ana pesa awape maskini wasiojiweza," alisema Pendo, akieleza kuwa baada ya kukataa, Mbuga alikata simu na hakupokea tena simu zake.
Pendo anasema alikaa kimya kwa siku nne kabla ya Machi 11, 2025, kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi Meatu kwa Afande Shafii.
Hata hivyo, licha ya kuahidiwa kupigiwa simu, hakupata mrejesho wowote. Aliporudia kuulizia maendeleo ya uchunguzi Machi 13, alijibiwa kuwa bado anatakiwa kusubiri.
Hali hiyo ilimfanya pia amtafute Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Meatu, ambaye naye alimtaka asubiri kupigiwa simu, jambo lililozidi kumpa mashaka juu ya usalama wake.
"Najiona nipo hatarini kwa sababu nimekataa mpango wa uhalifu wa mtu mwenye uwezo mkubwa wa fedha. Sijui kama baada ya kukataa, alifikiria nini juu yangu au kama tayari ameshatafuta watu wengine wa kutekeleza mpango huo," alisema Pendo huku akieleza hofu yake juu ya usalama wake.
Aidha, Pendo ametoa wito kwa Serikali, viongozi wa dini, na mashirika ya kutetea haki za binadamu kusaidia kuhakikisha usalama wake unalindwa na hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya wanaohusika.
Jambo TV tumemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Edith Swebe, ambaye amethibitisha kupokea taarifa hizo na kueleza kuwa uchunguzi bado unaendelea kutokana na unyeti wa tukio hilo.
chanzo. Jambo Tv