Polisi huko Lang'ata, Kenya wanachunguza tukio ambalo Faith Momanyi, binti mwenye umri wa miaka 19 aliyemaliza kidato cha 4, alifariki kwa kutatanisha nyumbani kwa mpenzi wake baada ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Faith inaripotiwa kuwa aliondoka nyumbani kwa wazazi wake, na katika kundi la watu watano, walienda kwanza kwenye sehemu ya starehe maarufu kando ya Barabara ya Lang’ata kwa ajili ya sherehe ya siku yake ya kuzaliwa, ambapo walikaa hadi saa 11 jioni.
Wakati kundi hilo likitawanyika, Faith alienda kwa mpenzi wake pamoja na rafiki yake mmoja wa kike. Dakika chache za usiku wa manane rafiki huyo wa kike aliwaacha Faith na mpenzi wake ndani ya nyumba hiyo.
Rafiki huyo anasema alijaribu kumtafuta Faith siku iliyofuata kuanzia asubuhi, lakini simu yake iliita bila kupokelewa, hadi saa kumi na moja jioni ambapo mpenzi wa Faith, Mark, alimpigia simu kumwarifu kuwa amefariki.
Majirani wanasema mpenzi wa Faith aliondoka kwenda kazini siku hiyo ya maafa, na alipokuwa akirejea nyumbani mwendo wa saa kumi na moja jioni, alikuta nyumba yake imefungwa. Kwa kutumia ufunguo wa ziada, aliifikia nyumba hiyo, na kumkuta Faith akiwa amekufa ndani ya nyumba hiyo.
Uchunguzi wa maiti uliofanyika kwenye mwili wa Faith unaonyesha kuwa alifariki dunia kutokana na kukosa hewa na kwamba kulikuwa na kiasi kikubwa cha maji kwenye mapafu yake. Sampuli zaidi zimewasilishwa kwa mkemia wa serikali kwa vipimo vya sumu.
Mpenzi wake bado yuko chini ya ulinzi wa polisi, Faith alipata alama ya B katika mtihani wa KCSE wa 2024 na alipaswa kujiunga na chuo kikuu mwaka huu, kulingana na wazazi hao