Mwili wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Multimedia (MMU) cha nchini Kenya, Sylvia Kemunto, aliyepotea kwa siku tatu, ulipatikana jana Jumatano usiku ndani ya tanki la maji, juu ya moja ya hosteli za chuo hicho.
Sylvia, mwanafunzi wa Mawasiliano ya Umma na Sayansi ya Kompyuta, alitoweka katika hali ya kutatanisha Jumapili, Machi 30, 2025. Mama yake, Triza Kwamboka, mkazi wa Kawangware, alituma pesa za matumizi kwa binti yake kupitia simu ya kiongozi wa kanisa. Alipojaribu kuthibitisha kama Sylvia amepokea pesa hizo, simu yake haikupatikana. Akiwa na wasiwasi, mama huyu alisafiri hadi chuoni na uongozi wa chuo ukathibitisha kutokuwepo kwa mwanafunzi huyo, hivyo mama yake akatoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Lang’ata.
"Sylvia aliniambia kuna kijana aliyekuwa akimtaka sana kimapenzi lakini yeye alikuwa hamtaki. Nilimshauri awe imara na makini na masuala ya mapenzi," anasema Kwamboka.
Uchunguzi umebaini kuwa boifrendi wa Sylvia, Philip Eric Mutinda, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Uhandisi wa Umeme, alifika chumbani kwake saa 7:00 mchana siku hiyo. Mashuhuda walimwona Mutinda akihangaika kubeba begi kubwa, linalodaiwa kuwa la Kemunto, akilitoka katika chumba cha msichana huyo ghorofa ya tatu hadi chumba kwenye chake kilicho Block E, namba 301.
Usiku huo, waliohijiwa wanasema begi lilionekana chumbani kwa Mutinda lilitoweka alfajiri.
"Tulipofanya uchunguzi, tuligundua kuwa simu ya Sylvia ilizimwa saa 4:00 usiku, siku ya kupotea kwake, huku ishara yake ya mwisho ikionyesha kuwa bado alikuwa ndani ya chuo," anasema Kaimu Makamu Mkuu wa MMU, Prof. Geoffrey Kihara.
Jumatano, harufu kali kutoka Block E iliwaelekeza walinzi wa chuo kwenye tanki la maji juu ya jengo hilo, ambako mwili wa Sylvia Kemunto ulipatikana ukiwa umeharibika vibaya.
Polisi wanamsaka Mutinda, ambaye ametoweka tangu tukio hilo. Familia ya Sylvia na wanafunzi wanataka majibu kuhusu jinsi mauaji ya msichana huyo yalivyofanyika bila yeyote kugundua.
Chanzo: Citizen Digital
See Translation