Jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Diana Edward Bundala (42) maarufu kama Mfalme Zumaridi mkazi wa mtaa wa Buguku kata ya Buhongwa kwa tuhuma za kuendesha shughuli za kidini bila usajili pamoja na kufanya mahubiri kwa waumini wake kwa sauti ya juu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema Mfalme Zumaridi pia anahojiwa kuhusiana na taarifa inayoendelea kusambaa katika mitandao ya kijamii akionekana kwenye picha mjongeo akiwa na kundi la watoto wenye umri mdogo wa jinsia ya kike na kiume akiwaeleza kuwa yeye ndiye Mungu wao ambaye ana uwezo wa kuwatenganisha na kifo.