Yohana Kilowoko mwenye umri wa miaka 37 mkazi wa mtaa wa sekondari uliopo kata ya Maguvani mjini Makambako wilayani Njombe amefariki dunia usiku wa kuamkia mei 26,2025,baada kulala na jiko la mkaa kwenye chumba ambacho amekuwa akifanyia biashara ya mahitaji ya nyumbani.
Akizungumza na kituo hiki mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa sekondari Nsangalufu Mwakasumbula amesema majira ya saa tisa usiku alipigiwa simu na majirani wa marehemu kuwa kuna ajali ya moto,ambapo mara baada ya kufika eneo la tukio licha ya kufanikiwa kuuzima moto huo bado wameshindwa kuokoa uhai wa Yohana kwani wamekuta ameshapoteza maisha.
Mwenyekiti huyo amesema mara baada ya kuuzima moto huo na kuingia ndani wamekuta jiko la mkaa kwenye chumba hicho ambacho marehemu alikuwa amelala kwaajili ya kulinda bidhaa za mahitaji mbalimbali ya nyumbani na kufafanua kuwa bidhaa hizo pia zimeteketea zote kwa moto.
Balozi wa eneo hilo Daina Sambala na baadhi ya majirani,Jema Longo na Salumu Tangwa wamesema walifika eneo la tukio baada ya kuona moshi mkubwa usiku,na kueleza kuwa jamii inatakiwa kuchukua tahadhali dhidi ya matumizi ya jiko la mkaa.
Oscar Kilowoko ambaye ni kaka wa marehemu Yohana Kilowoko amesema marehemu ameacha watoto wawili na mjane mmoja na kufafanua kuwa taarifa za tukio hilo amezipata kwa majirani wa marehemu.
Naye Mkaguzi wa jeshi la zimamoto na uokoaji Makambako David Ngulo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa baada ya uchunguzi wamebaini chanzo ni moto ambao umesababishwa na jiko la mkaa ambalo marehemu aliingia nalo kwenye chumba ambacho amekuwa akifanyia biashara za mahitaji ya nyumbani.