Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametumia muda wa dakika 166 (sawa na saa mbili, dakika 46 na sekunde 21) kutoa hotuba yake ya kuhitimisha Bunge la 12 kabla ya kuahirisha rasmi shughuli zake Juni 27, 2025.
Rais Samia amesema kuwa Bunge hilo limeahirishwa na kwamba litavunjwa rasmi Agosti 3, 2025.
Katika hotuba yake iliyojaa taarifa muhimu na takwimu, Rais Samia amezungumzia mafanikio ya Taifa, hatua zilizopigwa, changamoto na mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania kwa umahiri na uthabiti, akigusa sekta zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Bunge la 12 lilifunguliwa rasmi Novemba 13, 2020 na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Baada ya kifo chake, Rais Samia alilihutubia bunge hilo kwa mara ya kwanza Aprili 22, 2021, akieleza malengo na dira ya serikali yake pamoja na mafanikio ya awamu iliyopita.