Mbunge wa Jimbo la Geita Joseph Kasheku Musukuma ametaka Wageni wanaoalikwa Bungeni na Wabunge watambulishwe kwani kutambulishwa mbele ya Bunge ni heshima huku akisema Mbunge kuwapeleka Watu wake Bungeni ni moja ya ahadi ambazo wamekuwa wakitoa kwa Wananchi wanapokuwa wanatafuta kura.
Msukuma ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma June 11, 2025 wakati akichangia hoja kwa ya mabadiliko ya sheria na kanuni za Bunge za utambulisho wa Wageni “Kanuni ya 164(1)(2) ya Bunge imeeleza Watu watakaotambulishwa humu Bungeni, naona kama tunaenda kufanya ubaguzi kwa sababu hawa Watu waliotajwa kutambulishwa Spika anaweza kumtambulisha Mtu yeyote ambaye ameona amefanya kitu kikubwa kwenye nchi yake”
“Sasa tunapokuja humu ndani sisi Wabunge kuwaalika Watu waje Bungeni ni moja ya ahadi tunazozitoa wakati tunatafuta kura sasa jiulize Spika unamtoa Mtu kilometa zaidi ya 900 Geita unamleta Bungeni anapigwa baridi hapa halafu anamaliza anaondoka kama kundi la wanyama tuendelee kama tulivokuwa zamani kama suala ni muda wa kupumzika uongezwe kutoka saa saba kwenda saa nane kwasababu ni heshima Mtu kuja Bungeni”
Musukuma amesema hayo baada ya Kamati ya Kanuni za Bunge kusema utambulisho wa Wageni wanaohudhuria vikao vya Bunge unapoteza muda, hivyo imependekeza utambulisho ufanyike kwa Wageni mahususi wa kitaifa na kimataifa na wale waliotoa mchango wa kitaifa unaohitaji kuenziwa.