Mtu mmoja aliyekuwa akitafutwa kwa zaidi ya mwezi mmoja, Castory Madembwe, amepatikana akiwa ameuawa na kuzikwa kwa siri nyumbani kwa mtuhumiwa mmoja katika Mtaa wa Uledi, Kata ya Mpera, Manispaa ya Tabora.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Tabora, baada ya kumkamata mtuhumiwa, alikiri kumteka Castory, kumuua na kuufukia mwili wake ndani ya nyumba yake, kisha juu ya shimo hilo kutengeneza bustani ya nyanya ili kuficha ushahidi wa mauaji.
Mwenyekiti wa mtaa huo, John Peter, amethibitisha kufukuliwa kwa mwili huo leo, na kusema kuwa juhudi za Polisi kwa kushirikiana na wananchi ndizo zilizozaa matunda.
Hadi mwili unafukuliwa, hakuna ndugu wa marehemu aliyekuwa na taarifa rasmi kuhusu upatikanaji wa mwili wa Castory Madembwe. Polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo la kusikitisha.