Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Isaya Kastam mkazi wa Kwa Mfipa Kibaha kwa tuhuma za mauaji ya mpenzi wake, Faraja Chafu.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 8, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema kuwa tukio hilo limetokea Julai 7 saa tatu usiku Kibaha.
Polisi imedai kwamba mtuhumiwa alimshambulia mpenzi wake anayefahamika kwa jina Faraja Chafu Mkazi wa Kwa Mfipa kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za wake na kumsababishia majeraha.
Amesema kuwa chanzo cha kumshambulia mpenzi wake huyo ambaye ni marehemu kwa sasa, ni wivu wa mapenzi baada ya kutoelewana na kwamba alifariki wakati akiwahishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwa ajili ya matibabu.
"Baada ya kumshambulia kwa kisu mtuhumiwa alitoroka lakini baadaye alipatikana maeneo ya Kigamboni jijini Dar Salaam baada ya kujaribu kunywa kitu kinachodhaniwa kuwa ni sumu ili ajiue," amesema.