Mwanamke mmoja aliefahamika kwa jina la Getrude Silivesto miaka 38 mkazi wa kijiji cha Kaulolo Kata ya Nsekwa Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi amefariki dunia kwa kuchomwa na kitu kinachosadikiwa kuwa na ncha kali sehemu ya mbele ya sikio la kushoto na upande wa shingoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi SACP Kaster Ngonyani amesema tukio hilo la kusikitisha limetekelezwa na mme wake Talisiswusi Salvatory miaka 42.
Kamanda ngonyani amesema chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa kifamilia wa muda mrefu huku akibainisha tukio hilo limetokea Majira ya Saa Moja Asubuhi kuamkia Julai 2,2025.
Amebainisha kuwa tukio hilo limetekelezwa na mme wake huyo wakati mke wake akiwa amelala na kumchoma na kitu hicho chenye ncha kali.
Kwa mujibu wa Kamanda Ngonyani mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi hilo katika kituo cha polisi inyonga Wilala ya Mlele kwaajili ya mahojiano zaidi kuhususiana na tukio hilo na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.
Katika hatua nyingine Ngonyani ametoa wito kwa wananchi hususani wanafamilia wanapokuwa na changamoto za ndoa kutumia dawati la polisi la jinsia ambalo linahusika na masuala ya kifamilia pamoja na viongozi wa dini kwenye maeneo yao ili kuepusha kujichukulia sheria mkononi.