Rais wa Kenya atoa ruhusa wezi na waharifu kupigwa risasi

Adimin
0

Rais wa Kenya William Ruto, akiwa na hasira kali, ameapa kuwachukulia hatua kali wale anaowaita wapanga njama wa kutaka kumuondoa madarakani kwa njia zisizo halali kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.


Akizungumza Jumatano katika Kituo cha Polisi cha Kilimani jijini Nairobi baada ya kukagua mradi wa makazi ya maafisa wa polisi, Rais Ruto alisisitiza kuwa hatakubali vurugu kutumiwa kama njia ya kubadili uongozi wa taifa.

"Nataka kuwaambia hao wahuni wanaodhani wanaweza kuondoa serikali hii kwa vurugu na njia haramu kabla ya 2027, wajitokeze, wajaribu," alisema kwa ukali.

“Hii ni nchi ya kidemokrasia, uongozi wa taifa utachaguliwa kupitia kura ya wananchi, si kwa risasi au fujo,” aliongeza.

Rais Ruto alilalamikia kile alichokiita ni mashambulizi ya makusudi dhidi ya serikali yake kwa njia ya vurugu, akijiuliza kwa nini marais waliomtangulia hawakukumbana na hali kama hiyo.

“Wananisemea kuhusu Moi, Kibaki, Uhuru… hawa wote walikuwa marais, kwa nini wakati wao hakukuwa na fujo kama hizi? Mbona sasa? Upuuzi huu lazima ukome,” alisema Rais kwa ukali.

Katika hotuba hiyo ya kihisia, Rais aliapa kutumia "njia yoyote inayopatikana" kulinda usalama wa taifa na kuhakikisha wote wanaosababisha vurugu, ama moja kwa moja au kwa kuwafadhili, wanakabiliwa na mkono wa sheria.

"Tunataka amani Kenya? Tunataka watu wafanye biashara? so mtu ambaye anaenda kuchoma biashara ya mtu mwingine, mtu anayechukua moto anaenda kuchoma biashara ya mtu, anaenda kuchoma mali ya watu wengine, mtu kama huyo apigwe risasi miguu aende Hospitali, akienda Kortini, wasimuue lakini wapige hii miguu ivunjike. Hatuwezi kukubali mtu anaamka kwake anaenda kuchoma biashara na mali ya watu wengine, hii ni haki? huu mchezo watu waache. Niseme askari wasipige risasi wananchi kuua lakini muhalifu ashughulikiwe, apigwe risasi, aende Hospitali, akienda Kortini." Rais wa Kenya Willium Ruto leo Julai 09, 2025

Ruto aliitaja hali ya kushambuliwa kwa vituo vya polisi kama kitendo cha “kutangaza vita” dhidi ya taifa, akisema hawezi tena kuvumilia vitendo vya namna hiyo.

“Mtu yeyote anayeshambulia kituo cha polisi humu nchini, hiyo ni sawa na kutangaza vita. Hatutakubali. Inatosha sasa,” alisema kwa msisitizo. “Nitawalinda Wakenya na mali zao kwa gharama yoyote.”

Kauli hiyo ya Rais imekuja baada ya mfululizo wa maandamano yaliyoshuhudiwa nchini kote, ambayo yamesababisha uharibifu wa mali, mauaji ya waandamanaji, pamoja na tuhuma za kuingizwa kwa makundi ya wahuni waliodhaminiwa kisiasa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top