Mwanaume Lazaro Kidibule (36) ambaye pia alikuwa ni Mwalimu wa Chuo Cha Maendeleo ya Wanachi (FDC) Ulembwe kilichopo katika kijiji cha Usita, kata ya Ulembwe Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe amefariki dunia kwa kunywa sumu huku sababu ni wivu wa mapenzi.
Wakizungumza na Kings Fm baadhi ya Rafiki wa marehemu akiwemo Exavel Kayombo, Mstafa Bashee wamesema kuwa siku kadhaa nyuma walisikia kuwa Lazaro alikuwa na ugomvi na mke wake ingawa yeye hakuweka wazi juu ya changamoto zake hadi kufikia umauti.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho amesema kuwa alipata taarifa hizo kuwa Lazaro amekunywa sumu kutoka kwa mke wake ambapo alieleza kuwa alichukuliwa akiwa anatokwa na povu mdomoni kwenda kupata matibabu hayo.
"Nilikuwa nampgia simu Lazaro alikuwa hapatikani baada ya kuona hapatikani nikampigia mke wake na baada ya kuumiliza Lazaro yuko wapi alijibu yupo hospitali amekunywa sumu anaendelea na matibabu" ameongeza Mkuu wa chuo.
Galus Kawogo ni Mwenyekiti wa kijiji cha Usita amesema kuwa alipigiwa simu asubuhi na Afisa mtendaji wa kijiji hicho na kumpa taarifa kuwa kuna msiba wa mtu ambaye anasadikika amekunywa sumu ambapo mwenyekiti huyo alichukua jukumu la kwenda eneo la tukio.
Baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wamesema kuwa mwalimu huyo alikuwa msaada mkubwa kwako hasa katika kuwafundisha somo la ujasiriamali na maisha ya kujitegemea.