Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linawashikilia askari wawili wa Jeshi la Magereza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha kijana Emmanuel Lucas (18), mkazi wa Kijiji cha Kisangura, Wilaya ya Serengeti.
Tukio hilo lilitokea Machi 31, 2025, majira ya saa 10 alfajiri ndani ya kambi ya mradi wa ufugaji katika Gereza la Tabora B. Askari hao walikamatwa baada ya kudaiwa kufyatua risasi wakati wa mvutano na kundi la vijana waliokuwa wamevamia eneo hilo la mradi kwa lengo la kuchukua mifugo iliyokuwa imekamatwa kwa kuingizwa kinyume cha sheria kambini hapo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, askari hao walifyatua risasi hewani kwa lengo la kuwatawanya vijana hao, lakini moja ya risasi hizo ilimpata kijana Emmanuel Lucas, ambaye alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitalini.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kubaini mazingira halisi ya tukio hilo. Aidha, limewataka wananchi kuzingatia mipaka ya malisho ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.