Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema siku ya uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, chama hicho kitaitisha maandamano ya kuuzuia uchaguzi usifanyike.
Kauli hiyo ya Lissu, inajibu swali kuhusu mbinu ambayo chama hicho itaitumia kuzuia uchaguzi kuendana na ajenda yake ya ‘No Reforms, No Election’ (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi).
Lissu amesema hayo Aprili 7, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara katika ziara ya kutoa elimu kuhusu ‘No Reforms, No Election.’
Amesema iwapo Serikali haitafanya mabadiliko ya sheria na kanuni za uchaguzi, chama hicho kitawahamasisha wananchi kuandamana kuuzuia uchaguzi usifanyike.
“Hatutaenda kupiga kura, hatutaenda kujiandikisha, siku ya kupiga kura tutaandamana, watatufunga wote? Kuna sheria ya Tanzania inayosema lazima tushiriki kwenye chaguzi za kijinga?” amehoji.
Sababu ya hatua hiyo, amesema hawataki kwenda kwenye uchaguzi unaosimamiwa na wale walioharibu chaguzi za miaka iliyopita.
“Tutafanya kila linalowezekana kuhamasisha umma wa Watanzania kuzuia uchaguzi,” amesema.