Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kisihusishwe na vurugu zilizotokea wilayani Igunga, mkoani Tabora katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kukitaka chama hicho kikae kitafakari.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mji Mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi Vijijini,mkoani Kilimanjaro.
“Wenzetu leo (jana) wanahangaika, nimesoma hapa walikuwa Igunga mkutano sijui wamefanyiwa vurugu, nafikiri na nyie mmeona kwenye vyombo vya habari vurugu zimetibuka pale, lakini bila busara Makamu Mwenyekiti John Heche, ame tweet kwamba, ‘mkutano wetu vurugu hizi tumefanyiwa na vijana wa CCM’,” amesema.
Makalla amesema ameshangaa sana huku akisema kuna usemi wa Kiswahili unaosema, “kama kifaa ulichonacho ni nyundo usikariri kila tatizo ni msumari.
“Kama wewe umebeba nyundo usikariri kila tatizo linahusu msumari. Nataka nimwambie Heche kwamba, CCM kisihusishwe na tukio hilo.
"Ni tukio la kitoto, chama kikubwa kama Chama Cha Mapinduzi hatuwezi kushiriki tukio kama hilo. Heche aelewe CHADEMA siyo mshindani tena wa CCM kwa sababu katika uchaguzi huu hawashiriki uchaguzi. Sisi tuna maslahi gani na mkutano huo,” amesema.