Mahakama ya Tanzania imetangaza kuwa mashauri mawili ya jinai, namba 8606/2025 na 8607/2025, dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa, Tundu Antiphas Lissu, yanayotarajiwa kutajwa na kusikilizwa kesho Jumatatu tarehe 2 Juni 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, yatarushwa moja kwa moja (mubashara) kwa umma kupitia mitandao rasmi ya Mahakama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Gerard Julius Chami, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Mahakama ya Tanzania, uamuzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania unaolenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia katika huduma ya utoaji haki.
“Lengo la Mahakama kurusha mubashara matangazo ya mwenendo wa mashauri haya ni kuwawezesha wananchi popote pale walipo na ambao wanapenda kufuatilia mwenendo wa mashauri kuweza kufuatilia bila kuwa na ulazima wa kufika Mahakamani”, amesema Chami.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa chumba cha Mahakama ya Wazi Kisutu kina uwezo wa kuchukua watu 80* ekee, hivyo nafasi zitagawanywa kwa makundi ambapo kutakuwa na mawakili wa Serikali na watu wengine (10), Mawakili wa utetezi na watu wengine (60) na waandishi wa habari (10).
Kutokana na mahitaji ya matumizi ya ukumbi huo na Mahakimu wengine zaidi ya 10 wanaoendesha mashauri mengine, Mahakama inasisitiza wananchi wote wenye nia ya kufuatilia mashauri hayo kufanya hivyo kupitia njia za kidijiti.
Mahakama pia inawakumbusha wote watakaohudhuria mahakamani kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwa kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya yaliyotolewa kupitia taarifa rasmi ya tarehe 20 Mei 2025.
Mahakama inawahakikishia umma na Watanzania wote kuwa itaendelea kutoa haki kwa uwazi, kwa wakati na kwa wote. Tunawahimiza Wananchi wote kuendelea kushirikiana na Mahakama katika kujenga mfumo wa utoaji haki unaozingatia misingi ya Kikatiba, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali,” amesisitiza Chami.