WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa ametangaza tarehe ya kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani kuwa ni Juni 20, Mwaka huu kabla ya kuvunjwa kwa Bunge Juni 27,2025,ikiwa ni kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Tamko hilo amelitoa juni 15,2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tarehe kuvunjwa kwa mabaraza na mikutano ya kamati za kudumu za halmashauri.
Waziri Mchengerwa amesema baada ya hatua hiyo, masuala yote ya kiutendaji katika Halmashauri yatasimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mpito akisaidiana na Wakuu wa Idara kama wajumbe wa kamati.
"Mkurugenzi wa Halmashauri hataruhusiwa kuanzisha miradi au uwekezaji mpya, kubadilisha au kurekebisha mradi na uwekezaji au uamuzi wowote uliopitishwa na Halmashauri kabla ya kuvunjwa kwa kuwa atawajibika kisheria,"amesema.