Kufuatia wimbi la wananchi kujibu posti za viongozi wa Serikali na watu maarufu kwa kampeni ya No Reforms No Election inayotumiwa na CHADEMA, Msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema ni upuuzi akiwataka wajiepushe na kampeni zisizo na tija.
No Reforms No Election ni kampeni iliyoanzishwa na inayotangazwa kwenye mikutano ya CHADEMA wakitaka kuwepo mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi kabla ya kufika siku ya kupiga kura Oktoba 2025.
Katika mitandao ya kijamii makundi mbalimbali yanahamasisha kupaza sauti za kampeni hiyo kwa kuchapisha ujumbe na kutoa maoni ya No Reforms, No Election pale ukurasa fulani unapokuwa umechapisha maudhui yake yoyote.
Haijalishi ni ukurasa wa nani, iwe wa vyombo vya habari, kampuni, matangazo sehemu kubwa ya maoni ni No Reforms, No Election na wengine wanafupisha kwa kuandika NRNE.
Hali hiyo imewalazimu baadhi ya viongozi kuzima sehemu ya maoni ili kujiepusha na kampeni
Kauli ya Serikali
Alipoulizwa na tovuti ya Mwananchi Communications Ltd kuhusu hatua hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amejibu "Watu wameamua kufanya hivyo, tutafanyaje," amesema.
Ingawa katika maelezo yake aliwatahadharisha wanaofanya mchezo huo akidai hauna tija na 'upuuzi' zaidi ya kupoteza muda wao.
"Watu wajiepushe na kampeni zisizokuwa na tija, watumie mitandao kama fursa ya kujifunza teknolojia mpya, wanapaswa kutambua na kujua kutumia mitandao vibaya ni kupoteza rasilimali fedha kwa kuwa wanatumia bando," amesema.
Katika maelezo yake Msigwa amesema badala ya kupoteza muda kuendesha kampeni hizo watumie nafasi hiyo wajielekeze kujenga nchi yao.
"Kinachoendelea kwenye mitandao ni upuuzi. Huu ni upuuzi unaoendelea Watanzania wajielekeze kujenga nchi yao. Huwezi kuendesha kampeni ya kuzuia Uchaguzi wakati nchi imejiwekea kalenda yake," amesema Msigwa.
Kampeni hiyo imeenda mbali zaidi kwa kumgusa hadi msanii wa Nigeria Chellaboi ambaye amekuja nchini hivi karibuni na kushangazwa na ukurasa wake kumiminika maoni yanayohusu kampeni hiyo.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi